Wadau wakutana kujadili sheria ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Z'bar
Wadau visiwani Zanzibar wamekutana kujadili upungufu wWa sheria ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi ili kukusanya maoni na kuifanyia maboresho katika maeneo kadhaa kulingana na wakati uliopo sasa.
Mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Kurekebisha sheria kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC-Zanzibar) na chama Cha Mashirika yasiyo ya Kiserikali Zanzibar(Angoza) unajadili sheria namba moja ya mwaka 2012.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) Kamishina wa Polisi Makarani Ahmed amesema sheria hiyo tangu itungwe ina zaidi ya miaka 10 hivyo kuna maeneo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho.
"Kwanza kipindi cha nyuma hatukua haswa na sheria inayotaja rushwa moja kwa moja, tulikuja kupata sheria hiyo mwaka 2012 lakini ukianza kutumia kitu ndivyo unagundua changamoto na mahitaji," amesema na kuongeza
"Tunapozungumzia rushwa hatuwezi kupambana nayo sis wenyewe kama mamlaka peke yetu, lazima tushirikishe, asasi za kiaraia, vyombo vya habari na wadau wengine.
Amesema rushwa ipo ya aina nyingi, rushwa ya muhali, rushwa ya kawaida na rushwa kubwa inayohusu masula ya mikataba ambayo ndio mbaya zaidi na ngumu kushughulika nayo.
Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria, Mussa Kombo Bakari amesema yapo mambo mengi yanayotakiwa kuzingatiwa katika wakati wa kutengeneza sheria bora ikiwa ni pamoja na kuwahusisha wadau wengi katika maeneo hayo.
"Asasi za kiraia zinajikita kila sehemu, tunaweza kuhamasishana kuleta mabadiliko na tusisubiri kukumbushwa bali tuangalie maeneo yetu tupeleke ajenda serikalini nazo zitafanyiwa kazi.
Naye Mratibu wa THRDC-Zanzibar, Abdallah Abeid amesema
mifumo mizuri inatengenezwa kulingana na sheria bora.
Amesema washiriki wa mkutano huo pia wanatarajia kuangalia na kujifunza uzoefu wa nchi mbalimbali duniani katika kupambana na vitendo vya Rushwa na Uhujumu uchumi na namna Zanzibar inaweza kujifunza na kuboresha sheria hiyo kwa kutafuta mbinu mbadala, bora zaidi na zinazozingatia misingi ya haki za binadamu.
Comments
Post a Comment