Ulaya yataka hatua zaidi kupambana na omicron
Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Ulaya, ECDC kimeonya kuwa chanjo pekee haiwezi kuzuia kusambaa kwa aina mpya ya kirusi cha Omicron na kimetoa wito wa hatua zaidi kuchukuliwa kupambana na kirusi hicho.
Mkurugenzi wa ECDC, Andrea Ammon jana alielezea hatari iliyopo katika mfumo wa afya ya umma kutokana na kirusi hicho. Ammon amesema kirusi hicho kitakuwa kimesambaa zaidi ifikapo mwezi Januari au Februari. Kituo hicho kimependekeza kuwekwa vizuizi vikali na watu kufanyia kazi nyumbani pale inapowezekana ili kupunguza mzigo kwenye mfumo wa afya.
ECDC pia imetoa wito wa kuanzishwa tena amri ya watu kuvaa barakoa, kunawa mikono na kuweka vizuizi kwenye maeneo yenye msongamano wa watu.
Kamishna wa Afya wa Umoja wa Ulaya, Stella Kyriakides amesema kirusi cha Omicron ni kitisho kikubwa na kuna uwezekano kikasambaa zaidi mwanzoni mwa mwaka 2022.
Comments
Post a Comment