Majaliwa Atoa Maagizo Mazito Watu Wa Mapato
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi zote zinazokusanya mapato nchini zihakikishe zinaweka mipango endelevu itakayoziwezesha kusimamia matumizi ya mapato hayo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Alisema serikali imeendelea kusimamia taasisi zote zinazokusanya mapato na kuweka mifumo imara ya kusimamia matumizi yake.
Alitoa agizo hilo jana baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kampasi ya Mbeya. Mradi huo unajengwa katika Kata ya Iganzo jijini Mbeya na unagharimu Sh milioni 852.
Pia, Majaliwa alisema kuwa serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha inaweka mipango madhubuti na usimamizi sahihi wa biashara na wafanyabiashara ili waweze kunufaika zaidi na shughuli wanazozifanya.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alitoa wito kwa uongozi wa CBE uendelee kuweka mipango ya kuwafikia wafanyabiashara wa ngazi zote na hata wale ambao hawajaanza kufanya biashara ili kuwatoa woga wanapotaka kuanzisha biashara.
“CBE endeleeni kuweka mpango mzuri wa kuwafikia na kuwapa elimu ya biashara wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo ili kuwawezesha kufahamu namna bora ya kuzifanya biashara zikue zaidi na kuongeza tija,” alisema.
Alisema ili kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, serikali iliwaagiza viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana nao watafute maeneo mazuri na kuyawekea miundombinu muhimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Emmanuel Mjema alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu, ambapo chuo hicho kimetoa Sh milioni 502 na Serikali Kuu imetoa Sh milioni 350 kwa ajili ya ujenzi huo.
Alisema CBE, kampasi ya Mbeya ilianza mwaka 2013 ikiwa na wanafunzi 44 na sasa ina wanafunzi 947. Ongezeko hilo linaonesha kuwa chuo hicho kinaendelea kuaminika zaidi katika utoaji wa elimu ya biashara na ujasiriamali nchini.
Wakati huo huo, Majaliwa amefungua kiwanda cha Raphael Group cha kuongeza thamani zao la mpunga na mazao mengine kilichopo katika eneo la Uyole jijini Mbeya na kumpongeza mwekezaji huyo kwa hatua hiyo.
Aidha, Majaliwa alitoa wito kwa taasisi za serikali zinazojihusisha na sekta ya uwekezaji kutowasumbua wawekezaji bali wawaelimishe na kuwasaidia ili waweze kukuza zaidi shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Raphael Ndelwa alisema kampuni yao inafanyakazi kwa mfumo wa kilimo cha mkataba na wakulima zaidi ya 14,000 ambao kati yao 7,800 wamejiajiri katika kilimo cha mpunga na 5,800 wanalima maharage.
Comments
Post a Comment