Macron - Ufaransa, Ulaya kufungua ubalozi wa pamoja nchini Afghanistan
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema leo kuwa mataifa kadhaa ya Ulaya yanafanya kazi kufungua ubalozi wa pamoja nchini Afghanistan utakaowawezesha mabalozi wao kurejea nchini humo.
Akizungumza na wanahabari mjini Doha kabla ya kuelekea Jeddah nchini Saudi Arabia, Macron amesema hatua hiyo ya kisiasa ni tofauti mbali na kutambuliwa kisiasa au mazungumzo ya kisiasa na Taliban na kwamba watakuwa na uwakilishi pindi tu watakapofungua ubalozi huo huku akiongeza kuwa masuala ya usalama bado yanahitajika kutatuliwa.
Katika taarifa baada ya mazungumzo na Taliban wiki moja iliyopita, Umoja wa Ulaya ulipendekeza kuwa unaweza kufungua ubalozi hivi karibuni.
Marekani na nchi nyingine za Magharibi zilifunga balozi zao na kuwaondoa wanadiplomasia wao nchini Afghanistan baada ya kundi la Taliban kuchukua hatamu za uongozi nchini humo na kutangaza serikali ya mpito ambayo wanachama wake wakuu wako chini ya vikwazo vya Marekani na Umoja wa Mataifa.
Comments
Post a Comment