Jaji Mkuu awacharukia mawakili, wajibu

 


Wakati Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma akiwaonya mawakili wanaokiuka maadili ya taaluma yao kuwa muda wao umekwisha, baadhi yao wamesema hapaswi kuwatisha, bali anapaswa kushirikiana nao kutatua changamoto zilizopo.


Akizungumza wakati wa sherehe za kuwakubalia na kuwasajili mawakili wapya wa kujitegemea 313, zilizofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mkuu alisema baadhi ya mawakili wanashindwa kutambua kuwa wao ni maofisa wa mahakama na ni nguzo muhimu ya utetezi wa uhuru wa mahakama na kujenga imani ya wananchi kwa mahakama.


Alisema ni haki ya wakili kukosoa hukumu au uamuzi wowote wa mahakama na kwamba hata yeye anafurahi anapokosolewa, lakini kuna baadhi yao badala ya kukosoa uamuzi wa mahakama kwa haki, wamekuwa wakijificha nyuma ya majina bandia kwenye mitandao ya kijamii na kupotosha uamuzi wa mahakama.


“Wengine wanatumia mitandao ya kijamii kuwashambulia majaji na mahakimu kwa lengo la kuwafedhehesha na kuwadhalilisha. Unapochafua taswira ya mahakama, kumbuka unachafua taaluma yako ya uwakili,” alisema Jaji Juma na kuonya kwamba mawakili wa namna hiyo muda wao sasa umekwisha.


Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, mawakili wa kujitegemea, Francis Stolla, Timon Vitalis na John Seka walisema wanaunga mkono kauli na msimamo wa Jaji Mkuu Juma.


Walisema kuwa yapo majukwaa na taratibu sahihi za kukosoa hukumu au uamuzi wa mahakama na kwa lugha sahihi ya kiungwana isiyodhalilisha na wala si kumshambulia mtu, jaji au hakimu aliyetoa uamuzi husika.


Walisema kuwa kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na kutumia lugha za udhalilishaji kwa mtu binafsi ni kinyume cha maadili ya taaluma ya uwakili, si tu humdhalilisha aliyetoa hukumu bali huidhalilisha taaluma yenyewe.


“Jaji Mkuu yuko sahihi kwa sababu kwanza mitandao ya kijamii si jukwaa sahihi, bali kuna jukwaa sahihi la kukosa uamuzi,” alisema Vitalis.


Alisema uamuzi wa jaji au hakimu hukosolewa kwa njia ya rufaa na masahihisho kwa maana ya revision ambazo ndizo zinakubalika kisheria na si kwenda kwenye mitandao ya kijamii.


Aliongeza kuwa hata kama hukumu hiyo ina udhaifu mwingine ambao unaonesha uwezo mdogo wa mwandishi si sahihi kuiweka katika mitandao ya kijamii katika namna ya kumdhalilisha.


“Hayo si maadili ya kitaaluma na hilo ni jambo ambalo kwa sasa linataka kuzoeleka sana. Sawa mitandao ya kijamii inatumika kwa njia ya kupashana habari ili na mtu mwingine ajue msimamo wa mahakama, yaani kujua kilichojiri, mfano kuna magroup watu wanapeana hizo hukumu ili kupashana habari,” alisema na kuongeza:.


“Sasa hiyo inadhalilisha hata na taaluma yenyewe, haiishii tu kwa mwandishi. Unajua jamii wakati mwingine wanasema samaki mmoja akioza wote wameoza. Wanataaluma wanapaswa kulinda heshima ya wao wenyewe lakini pia kulinda heshima ya mahakama. Lakini sasa tunataka kutoka kwenye utamaduni wetu.”


Kwa upande wake Wakili Stola alisema kuwa wakili wa kujitegemea au wa Serikali ni ofisa wa Mahakama ya Tanzania na hata jaji ni ofisa wa Mahakama isipokuwa tu katika majukumu tofauti.


Alisema wakili ni ofisa ambaye amepewa mamlaka ya kumwakilisha na kumshauri mteja wake kama anaona kwamba hukumu imekosewa na kwamba ndiyo maana kuna mchakato wa kukata rufaa.


Rufaa yoyote ile maana yake ni kwamba hiyo hukumu huyo ambaye imemhusu anaona kwamba ina makosa kwa hiyo kuna utaratibu uliowekwa kwa kuikosoa au kuipinga hukumu ile.


“Huo ni utaratibu ambao ni rasmi. Lakini pia kuna utamaduni wa kitaaluma. Mtu anaweza kuandika makala jarida fulani akakosoa ile hukumu kitaaluma na ndiyo maana hata majaji wenyewe kwa mfano majaji wanaweza kuwa watatu, hukumu inapotolewa, mmoja wao akatofautiana na wengine,” alisema na kuongeza:


“Kwa hiyo mimi binafsi ninakubaliana na msimamo wa Jaji Mkuu kwamba sisi hasa wanasheria tuwe tunatumia lugha ambayo ni respective ya kitaaluma.”


Naye wakili Seka alisisitiza kuwa kukosoa hukumu kwenye mitandao ya kijamii si tatizo, bali tatizo ni lugha inayotumika na kumshambulia mtu binafsi badala ya uamuzi wenyewe.



Comments

Popular posts from this blog

NINATIBU KISUKARI, PRESHA, TEZIDUME, NGIRI NA NGUVU ZA KIUME

Uchaguzi wa rais nchini Libya uko mashakani

Mambo 8 yanayosababisha Gari kuwaka Moto na Jinsi ya kuyaepuka