Dk Mwinyi: Tutaimarisha Kikosi Cha Zimamoto
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema serikali itakiimarisha Kikosi cha Zimamoto ili kukabili athari za matukio ya moto kwenye hoteli za kitalii visiwani hapa.
Dk Mwinyi alisema hayo katika hafla ya uzinduzi wa hoteli ya kitalii ya Tui Blue Bahari Zanzibar iliyopo Pwanimchangani, mkoa wa Kaskazini Unguja. Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Sharif Ali Sharif alisema hoteli hiyo imefunguliwa baada ya ukarabati kutokana na ajali ya moto Januari 16, mwaka huu iliyosababisha uharibifu wa samani na baadhi ya majengo.
Dk Mwinyi alisema kumekuwa na matukio mengi ya moto katika hoteli za kitalii, hivyo serikali itahakikisha tatizo hilo linadhibitiwa kwani ina kila sababu kuunga mkono sekta ya utalii kwa kuwa ni nguzo ya uchumi wa visiwa hivyo. Alisema uwekezaji katika sekta ya utalii una manufaa matatu zikiwemo, ajira, wananchi kupata soko la kuuzia bidhaa na pia serikali kupata fedha kupitia kodi.
Dk Mwinyi alisema serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha sekta hiyo ili kuvutia watalii na ndio maana ikaingia mkataba na kampuni ya Adnata kutoka Dubai ili kuimarisha utoaji huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na kuunda kikosi cha utalii ili kuwahakikisha watalii usalama.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa alisema kurejea kwa huduma katika hoteli hiyo kunatokana na juhudi za mwekezaji kujitoa na kufanya kazi usiku na mchana. Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohmed Mahamoud alisema miongoni mwa mafanikio ya mkoa huo katika kukuza uwekezaji ni pamoja na kumaliza migogoro.
Sharif alisema Dola za Marekani 700,000 zimetumika kwa ajili ya kuweka vifaa vya kisasa vya usalama wa hoteli ili kujikinga na majanga kama hayo. Meneja wa hoteli hiyo, Eric Freinut aliipongeza Wizara ya Mambo ya Kale na Utalii kwa kuuunga mkono juhudi za kuifanyia matengenzo hoteli hiyo.
Comments
Post a Comment