Aliyenywesha Wanawe Sumu Ajieleza, Gwajima Amshangaa
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, amekielezea kitendo cha Veronica Gabriel cha kuwanywesha sumu watoto wake watano kwa kisingizio cha ugumu wa maisha kuwa ni ukatili mkubwa ambao serikali haiwezi kuuvumilia.
Naye mwanamke huyo, ameieleza kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita mazingira yaliyochangia hadi kufikia hatua hiyo. Veronica, mkazi wa Chato aliwanywesha sumu watoto wake hao watano juzi na wawili kati yao kufariki dunia kwa madai ya ugumu wa maisha. Watoto waliofariki ni Jane Mgema na Janeth Mgema.
Hata hivyo, watoto Grace Lemi, Grandi Manyama na Jane Mkama wanaendelea na matibabu. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Gwajima, vitendo kama hivyo vinaashiria uwepo wa migogoro ya kifamilia inayotokana na sababu mbalimbali ambazo hazipatiwi ufumbuzi mapema na jamii na kusababisha matatizo ya kisaikolojia kutokana na jamii kutokutekeleza wajibu wake wa kutunza na kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi ya familia.
Alibainisha kuwa wizara kwa kushirikiana na taasisi nyingine itaendelea kusimamia na kuhakikisha sheria za nchi zinatumika ipasavyo ili kuhakikisha wale wote wanaotenda vitendo hivyo wanachukuliwa hatua stahiki.
“Nawasisitiza maofisa Maendeleo na Ustawi wa jamii kuwa karibu na wananchi ili kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuweza kuzitatua kwa wakati ikiwemo kuwaelimisha fursa za kujikwamua kiuchumi na kuondokana na msongo wa mawazo utokanao na umaskini na sababu zingine,” aliagiza.
Aidha, alitoa rai kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutochukua hatua za kutoa uhai wa mwingine kwani ni kumnyima haki yake ya msingi ya kuishi.
Alisema serikali inatoa huduma ya msaada wa kisaikolojia na kijamii kupitia Maofisa Ustawi wa Jamii wanaopatikana katika Ofisi za Halmashauri, Hospitali za Wilaya na kwenye vituo vya mkono kwa mkono vinavyotoa huduma kwa wahanga wa vitendo vya ukatili ambavyo vipo katika baadhi ya hospitali za mikoa.
“Ninawaomba viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kimila pamoja na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika kuwaelimisha wananchi na kuwasaidia kufichua vitendo vya ukatili katika jamii na kubaini mapema viashiria vyake ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati,” alisisitiza.
Veronica Gabriel (30) anayetuhumiwa kuwanywesha sumu wanawe watano na kupelekea wawili kati yao kufariki dunia amesema kiini cha kufanya hivyo ni ugumu wa maisha.
Veronica alisema hayo juzi jioni mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ilipomtembelea katika Kituo cha Afya cha Kata ya Bwanga anapoendelea kutibiwa yeye na watoto wake watatu walionusurika.
Alisema ugumu huo wa maisha umechangiwa zaidi na baba wa watoto wake kumtelekeza na kushindwa kumhudumia hali iliyomuwia ngumu kwa kuwa kila mtoto ana baba yake.
“Nimefanya vibarua hadi nimechoka, hata nguvu zinaisha wakati mwingine, kuna siku nalala njaa, kwa kweli nilipoona mazingira yamenichosha, nikasema heri nife nipumzike. Kwa kweli niliona hata kama nikiacha watoto watateseka, kwa maana hata ndugu walishanitenga.
Nina kaka watatu walishanitenga, baba naye alishakamatwa, kwa kweli nilifikiria hata nikiwaacha watateseka tu, nikaona bora nife nao,” alisema.
Aliongeza: “Najua kwamba nimeshafanya kosa, ninachoomba hata kama wakinipeleka jela naomba tu wasinitese, kutokana na mateso niliyokuwa nayapata, naomba tu wanifunge lakini wasinitese.”
Veronica alisema muda mrefu ameishi maisha magumu na kumlazimu kutembea na wanaume tofauti ili apate fedha za malazi na chakula na sasa ana ujauzito wa miezi mitatu lakini aliyempa mimba hamfahamu.
Domitila Anthony, ndugu wa Veronica anayeishi Mwanza alisema walipotezana tangu mwaka 2000, hawakuwahi kuonana tena lakini baada ya kusikia taarifa ya tukio hilo aligundua aliyetenda ni ndugu yake ndio aliamua kumtembelea.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Bwanga, Dk Margret Kimwaga alisema uchunguzi umethibitisha watoto waliofariki na walionusurika akiwemo mama yao wote waliathiriwa na sumu na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe alisema baada ya uchunguzi kukamilika tayari mazishi ya watoto wawili waliofariki yameshafanyika na kuahidi kuwasaka wanaume wote waliotelekeza watoto kwani wao ndiyo kiini cha tukio hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuokoa maisha ya watoto watatu na kutoa wito kwa wanawake kuachana na ngono zembe ili kuepuka mimba zisizotarajiwa zinazopelekea kupata watoto wanaoshindwa kuwalea.
Senyamule aliagiza Waratibu wa Mfuko wa Kusaidia Kaya Masikini (TASAF) kufanya ufuatiliaji wa kina wa wanawake wanaopitia magumu kama Veronica ili waweze kuwasaidia na kuepuka matukio ya aina hiyo kujirudia.
Comments
Post a Comment