Uholanzi yatikiswa na usiku wa pili wa ghasia dhidi ya vizuizi vya Corona
Machafuko mapya yamezuka nchini Uholanzi dhidi ya hatua za serikali za kudhibiti virusi vya corona. Waandamanaji wamewarushia polisi mawe na fashifashi huku maandamano yakigeuka kuwa ya ghasia kwa usiku wa pili.
Maafisa wa kutuliza ghasia walikabiliana na makundi ya waandamanaji mjini The Hague. Maafisa watano wa polisi wamejeruhiwa na takriban watu saba wamekamatwa. Awali vurugu zilizuka katika mji wa bandari wa Rotterdam, ambapo watu watatu walijeruhiwa wakati polisi walipofyatua risasi na washukiwa 51 walikamatwa.
Maandamano ya amani yaliyohusisha maelfu ya watu wanaopinga mipango ya kuwazuia watu ambao hawajachanjwa kufikia maeneo fulani yalifanyika katika miji ya Uholanzi mapema Jumamosi, lakini hali ilibadilika na kugeuka kuwa vurugu. Uholanzi ilirejesha baadhi ya vizuizi Jumamosi.
Meya wa mji wa Rotterdam Ahmed Aboutaleb amekosoa vurugu hiyo huku serikali ikitaja machafuko hayo kuwa ya kuogofya.
Comments
Post a Comment