Total yaitega Serikali umeme wa jua, upepo
Wakati umeme unaozalishwa nchini ukipungua kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, Kampuni ya Total Energies imesema ipo tayari kuzalisha kiwango chochote cha umemejua na upepo kitakachoridhiwa, na Serikali imewakaribisha.
Ikizindua mwonekano mpya wa vilainishi vyake vinavyozalishwa nchini, kampuni hiyo kubwa ya nishati duniani ilisema kwa sasa ipo kwenye mazungumzo na Serikali kupitia Wizara ya Nishati juu ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia upepo na jua.
Mkurugenzi Mtendaji wa Total Energies Tanzania, Jean-Francois Schoepp alisema mpaka mwaka 2050 kampuni hiyo inalenga kuwa wazalishaji wakubwa wa nishati jadidifu duniani, kwani kadri siku zinavyozidi kwenda nishati hiyo inahitajika kwa wingi zaidi kupunguza hewa ya ukaa.
Akifafanua kuhusu mpango wa uzalishaji umeme nchini, Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Total Energies Tanzania, Getrude Mpangile alisema wana uwezo wa kuwekeza kiasi chochote kitakachokidhi mahitaji baada ya kukamilisha mazungumzo hayo na Serikali.
“Tayari Total Energies tunazalisha umeme katika mataifa tofauti duniani, husuani Ulaya, uzalishaji wetu zaidi unatokana na jua, upepo na jotoardhi na sasa ni wakati wa Tanzania tunaiona fursa kwenye jua na upepo,” alisema Getrude.
Mwanasheria huyo wa kampuni alieleza kuwa sasa hivi mazingira ya kuwekeza nchini yanavutia, ndiyo maana wapo tayari kufanya hivyo kusaidia kuiangaza Tanzania na kujenga uchumi imara wa viwanda utakaotumia nishati nafuu ila ya uhakika.
Bila kutaja kiwango cha uwekezaji na maeneo ya kipaumbele, Getrude alisema kampuni hiyo imefanikisha uzalishaji wa umeme katika mataifa mengi na sasa ni zamu ya Tanzania.
“Pindi mazungumzo ya awali yakikamilika, tutafanya upembuzi yakinifu kwa kuzingatia maafikiano,” alisema.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe aliyekuwepo katika uzinduzi huo aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwekeza nchini kwa zaidi ya miongo mitano, akisema uwepo wao umetoa uhakika wa upatikanaji wa bidhaa inazozalisha, ajira na mpango wao wa kuzalisha umeme utasaidia kupunguza tatizo lililopo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Leonard Masanja alisema Serikali ina nia ya kuwa na miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia jua na upepo na inawakaribisha wawekezaji hao kwa ajili ya majadiliano na siyo Total Energies pekee walioonyesha nia, ila wapo wengine wengi waliofanya hivyo.
“Kuanza kwa uwekezaji kama huo kunategemea makubaliano, hususan kwenye masuala ya kifedha kwa kuwa miradi kama hiyo ina miundo mingi. Wapo wanaotaka wazalishe umeme halafu waiuzie Tanesco, wapo wanaotaka waanzishe mradi kisha Serikali irudishe gharama kama mkopo na kuna wanaotaka mradi wa pamoja na Serikali,” alisema Masanja.
Alisema suala ni makubaliano na aina ya mkataba unaopendekezwa, mwekezaji anachopaswa kufanya ni kuainisha mpango wake na kuwasiliana na Tanesco na wizara kabla hajaonyeshwa maeneo ambayo uwekezaji wa aina yake unaweza kufanyika.
Kwa sasa, Total Energies inatekeleza mradi wa kuzalisha umemejua huko Al Kharhsaah nchini Qatar unaotarajiwa kuzalisha megawati 800 katika eneo lenye kilomita 10 za mraba kwa gharama ya Sh1 trilioni.
Mradi huo ambao upo umbali wa kilometa 80 kutoka Jiji la Doha unatekelezwa na Total Energies kwa asilimia 49 na Kampuni ya Marubeni kwa asilimia 49, na umeme utakaozalishwa katika mradi huo utakuwa ukiuzwa kwa Sh36.04 kwa uniti moja.
Kwa sasa nchini Qatar umeme huuzwa Sh75.90 kwa uniti moja (kWh) kwa matumizi ya majumbani na Sh82.80 kwa matumizi ya kibiashara, hivyo kuanza kwa mradi huo ambao utaweza kuhudumia mahitaji ya Taifa hilo kwa asilimia 10 huenda kukawapunguzia wananchi bei hivyo kuchochea kukua kwa uchumi.
Katika mradi huo, Shirika la Umeme na Maji nchini Qatar (QEWC) litamiliki asilimia 60 na asilimia 40 zitakazobaki zitamilikiwa na Total Energies na Marubeni ambayo ni kampuni ya Kijapani. Uwezo wa juu wa kuzalisha umeme unatarajiwa kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2022.
Mradi mwingine unaotekelezwa na kampuni hiyo ni wa upepo uliopo huko nchini Scotland ukiitwa Seagreen Offshore Wind Farm ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 1,500 unaotekelezwa kwa thamani ya Sh9.21 trilioni. Mradi huo unatarajiwa kuzinufaisha kaya milioni moja na utaanza mwaka 2022 na ukikamilika utakuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya umeme wa upepo iliyopo kando ya bahari.
Comments
Post a Comment