Serikali Kushirikiana Na Singapore Kuboresha Bandari

 


MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Tanzania itashirikiana na uongozi wa Bandari ya Singapore kutoa mafunzo kwa watumishi wa bandari za Tanzania.


Dk Mpango alisema wataalamu wa bandari kutoka Singapore watakuja Tanzania kushirikiana katika kufanya maboresho ya haraka hasa Bandari ya Dar es Salaam. Alisema hayo alipotembelea bandari ya nchi hiyo na kujionea namna inavyofanya kazi.


Dk Mpango alisema mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano umedhamiria Tanzania iwe kituo kikuu cha biashara kwa kupitisha mizigo ya ndani ya nchi na nchi zote zinazoizunguka kwa kupitia bandari.


Alisema ushirikiano na Singapore kuboresha bandari za Tanzania Bara na Zanzibar kutaongeza kasi katika utekelezaji wa mpango huo. Katika ziara hiyo, Dk Mpango alishuhudia teknolojia zinazotumika kufanya kazi katika bandari hiyo ukiwemo upakuaji na upakiaji makasha na mizigo, ukaguzi wa mizigo na ufuatiliaji makasha yanapokuwa safarini.


Makamu wa Rais wa Mamlaka ya Bandari ya Singapore anayeshughulikia masuala ya biashara, Ong Seow Leong alisema bandari hiyo imewekeza katika mafunzo na ubunifu uliowezesha kuongezeka kwa teknolojia inayotumika sasa katika kutoa huduma ikiwemo kushusha na kupakia makasha 150,000.


Leong alisema bandari ya Singapore imekua na mtandao na bandari nyingine duniani hivyo kuongeza ufanisi wa ufanyaji kazi wa bandari hiyo.



Comments

Popular posts from this blog

NINATIBU KISUKARI, PRESHA, TEZIDUME, NGIRI NA NGUVU ZA KIUME

Uchaguzi wa rais nchini Libya uko mashakani

Mambo 8 yanayosababisha Gari kuwaka Moto na Jinsi ya kuyaepuka