NATO yasema inafuatilia shughuli za kijeshi za Urusi kwenye mpaka na Ukraine
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema wanafuatilia kwa karibu ongezeko la idadi ya wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wa Ukraine na kuionya Moscow dhidi ya matendo yoyote ya kichokozi.
Akizungumza na waandishi habari mjini Brussels akiwa pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dmytro Kuleba, Stoltenberg amesema jumuiya ya NATO inatizama kwa umakini kile kinachofanywa na Urusi kwenye eneo hilo.
Katika wiki za hivi karibuni Urusi imeongeza shughuli za kijeshi kwenye mpaka wake na Ukraine lakini Moscow imesema haina sababu ya kujieleza pale inapoamua kuhamisha wanajeshi kutoka sehemu moja hadi nyingine ndani ya mipaka yake.
Serikali ya Ukraine imesema ni muhimu kwa washirika wa Ulaya na Marekani kuchukua hatua kudhibiti vitendo hivyo vya Urusi ikitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea mzozo mpya wa kijeshi utakaokuwa na gharama kubwa zaidi.
Comments
Post a Comment