Mfahamu mwanamziki Fally Ipupa kiundani zaidi

 


Desemba 14, 1977 alizaliwa mwanamuziki, mtanashati kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) Fally Ipupa.

Jina lake halisi ni Fally Ipupa N'simba. Alizaliwa jijini Kinshasa kwa baba Faustina Ebamba Ipupa na mama Monique Bolutuli Mbo.

Mzee Faustin alikuwa na watoto wengine watatu, Bony Liston, Tyna Ipupa pamoja na Niclette Ipupa.

Kuanzia mwaka 1992 hadi 1993, Ipupa alianza kuupenda muziki na kuamua kushirikiana na vijana wenzake, Sankara Dekunta, Atele Kunianga na Pitshou Luzolo, ambapo walianzisha bendi yao waliyoiita ‘Flahs Success’ kwenye mtaa wao ndani ya Manispaa ya Bandalungwa (Bandal).

Mwanzoni wazazi wake hawakupenda ajishughulishe na muziki, walimtaka ajikite zaidi kwenye elimu, kwani walipenda Ipupa awe daktari.

Mwaka 1995, Ipupa aliachana na bendi hiyo na kujiunga na bendi ya Kibinda Nkoy iliyokuwa na maskani yake katika Manispaa ya Kintambo.

Hapo alikutana na mwanamuziki, Segun Mignon (Maniata) ambaye amewahi kufanya kazi na mjomba wake, JB Mpiana katika bendi ya Wenge Musica BCBG.

Hata hivyo, Ipupa hakudumu sana kwenye bendi hiyo, ambapo yeye na Maniata waliamua kuunda bendi nyingine waliyoiita Nouvelle Alliance, ikimaanisha muungano mpya.

Katika bendi hii ndipo Ipupa alipoanza kupata umaarufu hasa katika uimbaji, unenguaji pamoja na kurapu (atalaku).

Mwaka 1997, Ipupa alijiunga na bendi ya Quarter Latin ya Koffi Olomide (Le Grand Mopao Mokonzi), hapo alisafiri na bendi hiyo kwenda nchini Ufaransa na kufanya shoo iliyofanyika jijini Paris kwenye Ukumbi wa Bercy.

Albamu ya kwanza akiwa na Koffi Olomide iliitwa ‘Attentant’ na baadaye alishiriki katika albamu ya ‘Force De Frape’, ambapo aliimba wimbo uitwao ‘Eternellement’ ukiwa ni utunzi wake wakati huo akiwa umri wa miaka 15.

Mwaka 2001, ilipotoka albamu ya “Efrakata’, Koffi Olomide alimpa nafasi kubwa ya kuimba kuliko waimbaji wote, alishiriki kuimba karibu nyimbo zote, pia alionyesha uwezo mkubwa wa kurapu kwenye wimbo wa ‘Generation Bercy’.

Pia, wawili hao waliimba pamoja kwenye wimbo uitwao “Effervescent’ na hata kwenye video ya wimbo huo walionekana wamevaa sare.

Koffi aliamua kumteua Ipupa kuwa kiongozi wa bendi badala ya Felly Tyson.

Mwaka 2003, ilipotoka albamu ya ‘Affaire D’Etat’, Ipupa alipewa fursa ya kuimba peke yake kwenye wimbo wa ‘Ko-ko-ko’ (Hodi) ambao ni utunzi wake.

Mwaka mmoja baadaye, baada ya kutoka albamu ya ‘Monde Arab’ (Dunia ya Waarabu), alipewa kipaumbele cha kuimba nyimbo zote zikiwemo Esili (Imeisha) na Eputsha.

Kuanzia hapo jina la Fally Ipupa lilianza kukua kwa kasi ndani na nje ya DRC.

Baadaye, Ipupa alipata wazo la kujitegemea baada ya kuona anamudu vizuri kuimba, kutunga, kunengua na hata kurapu.

Fikra zake zilikuwa ni kutoa albamu yake mwenyewe na ndipo alipoanza kununua nyimbo mbalimbali kwa watunzi na kuchanganya na zake, huku akisubiri muda mwafaka kutangaza hadharani nia yake.

Mwaka 2005, ulitolewa wimbo uitwao ‘Boma nga na Elengi’ (Niue kwa utamu) huku yeye akishiriki kikamilifu.

Muda mfupi baadaye wakiwa kwenye maandalizi ya kutoa albamu ya ‘Danger De Mont’ (Hatari ya kifo), ndipo Ipupa alipoweka wazi nia yake ya kujitegemea na kumwambia Koffi Olomide kuwa anataka asimame mwenyewe.

Kwa upande wake, Koffi hakukubaliana na jambo hilo, hali iliyosababisha mtafaruku mkubwa huku wapambe wake na wale wa Koffi wakiingilia kati ili kuweka mambo sawa.

Wapambe wake wakamshauri ajiondoe kwa Koffi kama atakataa ombi lake la kutoa albamu nje ya bendi.

Baadaye ombi lake lilikubaliwa japo wanamuziki wengi hawakupenda hasa waimbaji. Waliokubali na kumuunga mkono ni Modogo Abarambwa na Montana Kamenga na baada ya hapo, Ipupa alienda kwenye Televisheni ya Taifa na kutangaza kuwa anatoa wimbo wa ‘Associe’ utakaokuwa kwenye albamu yake mpya.

Mwaka 2006, mkali huyo alijiunga na Lebo ya ‘Obouo Music’ inayomilikiwa na David Monsoh raia wa Ivory Coast na bila kukawia akatoa albamu ya kwanza iitwayo ‘Droit Chemin.’

Albamu hiyo ilikubalika sana kwenye soko la muziki na kupelekea kupata tuzo ya dhahabu mwaka mmoja baadaye.

Mwaka 2009, alitoa albamu iitwayo ‘Arsenal Des Belles Melodies’ na baada ya miaka minne, akafyatua nyingine iitwayo ‘Power Kosa Leka’.

Mnamo mwaka 2007 Fally Ipupa alishinda tuzo ya Kora kwa msanii bora kutoka Afrika ya Kati. Mnamo mwaka 2010 Ipupa alishinda tuzo ya MTV Africa kwa video bora ya Sexy Dance pia Msanii bora kutoka Ukanda wa Wazungumzaji wa Kifaransa. Pia litwaa tuzo ya Urban kwa kuwa msanii bora wa Kiafrika.

Ipupa alishiriki katika tuzo za MTV Africa mnamo mwaka 2014 katika kategori ya Best Live Act. Mnamo mwaka 2013 aliachia albamu ya Power ‘Kosa Leka’, katika albamu hiyo alitambulika sana kutokana na kupiga gitaa.


Comments

Popular posts from this blog

NINATIBU KISUKARI, PRESHA, TEZIDUME, NGIRI NA NGUVU ZA KIUME

Uchaguzi wa rais nchini Libya uko mashakani

Mambo 8 yanayosababisha Gari kuwaka Moto na Jinsi ya kuyaepuka