Merkel na Macron watafuta suluhu mzozo wa wakimbizi kwenye mpaka wa Poland na Belarus
Viongozi wa mataifa ya Ulaya jana wametanua juhudi za kidiplomasia kujaribu kutuliza mzozo kwenye mpaka kati ya Poland na Belarus ambao umewaacha maelfu ya wakimbizi wakiwa wamekwama kwa wiki kadhaa.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alifanya mazungumzo ya nadra na rais Alexander Lukashenko wa Belarus yaliyonuwia kutafuta njia za kutuliza hali iliyopo pamoja na msaada wa kiutu kwa wakimbizi waliokwama kwenye eneo hilo.
Kwa upande mwingine rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin ambaye ni mshirika wa karibu wa rais Lukashenko wakilenga kutanzua mzozo wa wakimbizi unaozidisha shinikizo kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya.
Umoja huo unailaumu serikali ya Lukashenko kwa kuwavutia wakimbizi kutoka mashariki ya kati na kuwasafirisha hadi kwenye mpaka na Poland kama sehemu ya kuiadhibu kanda hiyo kwa vikwazo ilivyoweka dhidi ya Belarus kutokana madai ya udanganyifu kwenye uchaguzi wa mwaka uliopita.
Comments
Post a Comment