Mbarawa awatumia salamu vigogo wa mizani, asema siku zao zinahesabika
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka wasimamizi na wafanyakazi wa mizani katika maeneo mbalimbali ya barabarani kujitafakari kuhusu mienendo yao ya utendaji kazi, akisema siku zao zinahesabika.
Waziri huyo amesema licha ya Serikali kufunga mifumo ya kamera za CCTV bado kumekuwa na malalamiko ya vitendo vya rushwa kwa watumishi katika mizani zilizoko maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa iliyotolewa na wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeeleza kuwa Profesa Mbarawa ametoa angalizo hilo wakati akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) katika makao makuu Dar es Salaam.
"Ni aibu na ni jambo la hovyo mtumishi wa mizani anaenda kuchukua rushwa hadharani na hajali uharibifu unaoendelea wa barabara zetu.
Huu ni mtandao unaoendelea kuanzia chini hadi juu, nawaambia na kuwatahadharisha kuwa siku zenu zinahesabika na nitawatoa siku za karibuni", amesema Profesa Mbarawa.
Profesa Mbarawa amewataka Tanroads kutoa elimu ya kutosha kwa wasafirishaji wote nchini ili kuwasaidia kufahamu haki na wajibu wao katika kusaidia kulinda miundombinu ya barabara na kupunguza malalamiko ya mara kwa mara.
Pia amemtaka Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatius Mativila kuhakikisha barabara kuu zinazounganisha mikoa yote nchini zinawekwa vivuko vya waenda kwa miguu au madaraja ya juu katika maeneo yanayostahili ili kupunguza idadi ya vifo vya watumiaji wa barabara.
Awali akitoa taarifa kwa waziri Mbarawa Mativila, amesema mueleza katika mwaka wa fedha 2021/22 taasisi hiyo, imejipanga kutekeleza miradi yote ya kimkakati kwa wakati na ubora unaotakiwa huku Sh897.656 bilioni ikimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Sh567.342 bilioni zitatumika katika matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo sehemu korofi na matengenezo ya madaraja," amesema Mativila.
Comments
Post a Comment