MAT yachunguza athari wanafunzi kubebeshwa mabegi ya uzito mkubwa
Wakati Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kikieleza kupokea malalamiko ya wanataaluma wake juu ya baadhi ya shule kuhatarisha afya ya watoto kwa kuwabebesha mabegi mazito, wadau wa elimu, madaktari na wazazi wametoa maoni juu ya malalamiko hayo.
Miongoni mwa malalamiko hayo mbali na watoto kubeba mabegi mazito, wengine hulazimishwa muda wa ziada wa kujisomea, mrundikano wa wanafunzi katika mabasi ya shule na wengine kupewa adhabu za masimango wanaposhindwa kupata alama A au B.
Mengine ni shule kutokuwa na viwanja vya michezo na watoto kulazimishwa kumaliza chakula hata kama ni kibaya au kapewa kingi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Rais wa MAT, Dk Shadrack Mwaibambe alisema chama hicho kina jukumu la kuishauri Serikali juu ya masuala ya afya yanapojitokeza.
“Hivyo, sasa tunachofanya ni kukusanya malalamiko baada ya hapo tutafute scientific evidence (ushahidi wa kisayansi) juu ya hayo kabla ya kutoa ushauri,” alisema Dk Mwaibambe.
Katika taarifa yake ya ndani iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii juzi, MAT inaeleza kuwa uzito wa mabegi hayo unasababishwa na kubeba madaftari na vitabu vya masomo yote kwa pamoja, jambo linaloweza kuwasababishia watoto matatizo ya mgongo katika umri mdogo.
Pia, taarifa hiyo imesema watoto wamekuwa wakilazimishwa kusoma kwa muda wa ziada wa kuanzia saa 11 alfajri hadi saa 1:30 asubuhi na saa 10 jioni hadi saa mbili usiku.
“Watoto kulazimishwa kukaa bweni hususan wa madarasa ya mitihani, la nne na la saba, na kupewa adhabu, kusimangwa wasipopata alama B na A kwenye mitihani. Usafiri wa shule kutozingatia umri na kujaza wanafunzi. Mtoto wa elimu ya awali anapanda basi moja na madarasa ya mbele yake hadi la saba,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Akizungumzia masuala hayo, mdau wa elimu nchini, Geofrey Telli alishauri kuwa badala ya shule kuweka nguvu kwa madarasa ya mitihani kwa kuwaweka kambi na bweni ni vyema wanafunzi ambao wana uelewa mdogo wapewe kipaumbele ili waweze kuinuka kulingana na wengine.
Alisema tofauti na hapo ni kumrundikia mwanafunzi vitu vingi kwa ajili ya kufaulu mitihani na si kwa ajili ya uelewa na kujifunza.
“Shule zinatakiwa kumfundisha mwanafunzi kufikiri, kutafakari na kufanya maamuzi, lakini sasa shule zimejikuta zinatoa mambo mengi kwa muda mfupi ili wanafunzi waweze kufaulu mtihani.
“Wanafanya hivyo kwa ajili ya biashara kuwa watapata wanafunzi wengi,” alisema Telli.
Kuhusu wanafunzi wanaobebwa na magari ya shule, alisema mbali na kurundikwa wengi, baadhi ya shule zimekuwa na magari machache, jambo linalofanya kuwepo kwa mzunguko mkubwa na wa muda mrefu.
“Shule ina gari moja, inakusanya wanafunzi sehemu nyingi, hivyo inalazimika kuanza mapema, mwanafunzi wa kwanza atapitiwa saa 10:30 alfajiri ili mzunguko uwahi kuisha na wafike shuleni saa mbili. Anaamka kabla ya huo muda, anafika shuleni yuko hoi,” alihoji Telli.
Kuhusu mzigo wa madaftari, alisema wanafunzi wadogo wanatakiwa kufundishwa masomo machache na muda mwingi uwe katika michezo, huku akibainisha kuwa kumrundikia masomo hakumfanyi kuelewa.
Alisema hilo huweza kufanya mwanafunzi kusahau hata majina ya masomo kutokana na wingi wake na kukariri walimu.
“Akifeli mnaanza kumgombeza, mnamvisha vinyago na kumsema vibaya, hii inaathiri hata baada ya kumaliza shule,” alisema Telli.
Akijibu hoja hizo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa shule binafsi Tanzania (Tamangosco), Leonard Mao alisema wakati mrundikano katika magari ukiangaliwa kwa nini ule wa madarasani ambao wanafunzi hukaa kwa muda mrefu zaidi hautupiwi macho.
“Wanafunzi wako wengi katika gari lakini wanatumia muda mchache kufika shuleni na kukaa kwa umbali, vipi kuhusu wanafunzi zaidi ya 200 wanaokaa darasa moja kwa saa zaidi ya nane,” alihoji Mao.
Kuhusu wanafunzi wa darasa la awali kuchanganywa na madarasa ya juu ndani ya gari la shule, alisema wasimamizi wa magari hayo huwa wako makini.
“Haina mantiki, zaidi ya msimamizi atawapanga hawa wakae viti hivi na hawa wakae viti hivi, kuna ubaya gani, kikubwa ni mkubwa asijekumkalia mdogo,” alisema Mao.
Akijibu juu ya kile kinachobainishwa kuwa ni kuwalazimisha wanafunzi wa madarasa ya mitihani kukaa bweni, alisema lengo ni kuwapatia muda wa kujisomea zaidi, kusoma masomo ya ziada ili waweze kufaulu masomo yao.
Khaji Nasibu, mmoja wa wazazi waliozungumza na Mwananchi alisema wakati mwingine ubora wa shule ndio hufanya wazazi kutozingatia vitu vingine vinavyoweza kumuathiri mwanafunzi.
Hilo huwafanya wazazi kuwapeleka watoto shule ambazo zinafanya vizuri bila kujali iko umbali kiasi gani na itamuathiri vipi mtoto.
“Mtoto kila siku yeye wa kwanza kuchukuliwa wa mwisho kurudishwa, akifika nyumbani akioga tu anasinzia, atapata wapi muda wa kujisomea,” alihoji Nasibu, huku akishauri kuwa ni vyema watoto wapelekwe shule za karibu na makazi yao.
Verdiana Anselmo, mzazi mwingine, naye aliziomba shule kuzingatia ratiba za masomo ili wanafunzi wabebe madaftari kwa ratiba.
“Hii ya kuwabebesha madaftari yote inawaumiza kwa kweli, mimi begi la mtoto wangu ukilinyanyua hata mtu mzima lazima ugune maana ni zito, sasa yeye yupo nalo muda wote unafikiri anaumia kiasi gani,” alisema Verediana.
Katika hilo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Magonjwa ya Ajali wa Taasisi ya Mifupa (Moi), Dk Kennedy Nchimbi alisema watoto wamekuwa wakiathiriwa zaidi migongo wanapobeba mabegi hayo.
“Tumekuwa tukipokea kesi nyingi za watoto wanaoingia kidato cha kwanza kuumwa migongo kwa sababu wanabeba mizigo mizito huku nyuma na unafika wakati mwili unashindwa kuvumilia,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema hilo huwaathiri sana watoto ambao miili yao haishughulishwi kuliko wale wanaojishughulisha, huku akisema utafiti utakaofanyika kupitia MAT utakuwa na majibu ya kina.
Comments
Post a Comment